United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office Labour,Employment,Youth and People with Disability

WIZARA YA KAZI NA AJIRA YATILIANA SAINI MAKUBALIANO YA AWALI YA USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA AJIRA NA NCHI YA QATAR

Ujumbe wa Serikali ya Qatar ukiongozwa na Mhe. Zayed bin Rashid Al-Nayemi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, ulitiliana saini makubaliano ya awali ya ushirikiano katika masuala ya ajira na Serikali ya Tanzania.

Katika kikao cha mashauriano baina ya nchi hizi mbili, kilichofanyika tarehe 25 Septemba, 2012 makao makuu ya Wizara ya Kazi na Ajira ambapo ujumbe wa Serikali uliongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Bwana Eric F. Shitindi.

Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano ya awali, Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Bwana Eric F. Shitindi alieleza kuwa makubaliano haya yataimarisha juhudi za Serikali za kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.

Aidha, kiongozi wa ujumbe wa Qatar, Bwana Zayed bin Rashid Al-Nayemi alisema makubaliano haya waliyotiliana saini yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Chini ya makubaliano haya ya awali, wafanyakazi watakaokwenda kufanya kazi nchini Qatar, watalindwa na Mkataba wa ushirikiano uliotiwa saini na nchi hizi mbili ambapo pia kutakuwepo na Tume ya Ushirikiano itakayoundwa na wajumbe kutoka nchi hizi mbili itakayosimamia makubaliano haya.

Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania ulikuwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Kiuchumi na Ushirika Zanzibar, Bibi Asha Ali Abdullah, Kamishna wa Kazi, Bwana Saul Kinemela, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira, Bibi Marietha Mcha, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kazi, Wizara ya

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bwana Christopher Mvula,Bw Eliezer Mwasele,Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za ajira Tanzania(TaESA) pamoja na wataalam mbalimbali kutoka Serikalini.

Kwa upande wa Serikali ya Qatar, ujumbe huo uliwashirikisha Mshauri wa Masuala ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dk. Reyadh Al Qaysi, Mkurugenzi Msaidizi masuala ya Sheria Wizara ya Kazi Qatar, Mwanasheria Wizara ya Kazi Qatar, Bwana Ali Al-Hadhrami na Bwana Ali Al-Bader kutoka Wizara ya Mambo ya Nje Qatar. Makubaliano haya ni rasimu ya mkataba wa ushirikiano ambapo unatarajiwa kutiwa saini hivi karibuni baina ya Mawaziri wa nchi hizi mbili. Nchi ya Qatar ni mojawapo ya mataifa yanayofanya nchi za Ghuba za Arabuni na ina utajiri mkubwa wa gesi na mafuta na hivi karibuni ilichaguliwa kuandaa mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia mwaka 2022.